Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan, juzi Jumapili tarehe 23 Farvardin 1404 (12 April 2026), kupitia tamko lililotolewa, limelaani vikali shambulio la hivi karibuni dhidi ya raia wa Kishia katika wilaya ya Injil, jimbo la Herat, na kulichukulia kuwa ni mfano wa kuendelea kwa vitendo vya vurugu dhidi ya jamii ya Kishia nchini humo. Baraza hilo limeitaka serikali iwabaini wahusika wa tukio hilo na kuwafikisha katika mahakama ya wazi.
Katika tamko hilo imeelezwa kuwa; shambulio la siku ya Ijumaa, tarehe 21 Farvardin (10 April 2026), lilifanywa na watu wenye silaha mchana kweupe, ambapo idadi ya wananchi, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, waliuawa kishahidi na wengine kujeruhiwa. Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan, pamoja na kutoa pole kwa familia za wahanga, limewaombea mashahidi maghfira na majeruhi kupona haraka, na limetahafharisha juu ya uwezekano wa kurudiwa kwa mashambulizi kama hayo.
Baraza hilo pia limesisitiza kuwa hapo awali, wahusika wa mashambulizi yanayofanana na hayo hawajafikishwa mahakamani hadharani, na jambo hili limechangia kuendelea kwa mzunguko wa vurugu nchini humo. Katika tamko hilo, serikali na vyombo vya usalama vimetakiwa kuhakikisha usalama wa raia na kuzuia kutokea kwa matukio kama hayo.
Hapo awali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan ilikuwa imetangaza kuwa; katika shambulio hilo takriban watu saba waliuawa kishahidi na wengine 13 kujeruhiwa. Hata hivyo, vyanzo vya ndani vimeripoti kuwa miili 12 imepelekwa katika hospitali ya kanda ya Herat na takribani watu 20 wengine wameathirika.
Shambulio hilo lilitokea siku ya Ijumaa tarehe 21 Farvardin (10 April 2026) saa 15:00 katika kijiji cha Deh-Miri, jimbo la Herat.
Maoni yako